Social Items

PropellerAds

MBINU ZA KUONGEZA MAUZO YAKO

MBINU TANO ZA KUONGEZA MAUZO YAKO KATIKA BIASHARA.
Leo tutaangalia eneo muhimu sana la kuhakikisha mzunguko wa fedha kwenye biashara yako unakuwa mzuri. Eneo hili ni mauzo. 
Mauzo ndio yanaleta fedha kwenye biashara yako na hivyo kama ukiongeza mauzo maana yake unaongeza fedha zinazoingia. Japokuwa hili halimaanishi kwamba ukiongeza mauzo umeongeza faida, la. Tutaangalia kwenye makala zijazo jinsi ya kuhakikisha unapata faida ya kukutosha. Leo tuangalie kwanza kuhusu mauzo ya biashara yako na jinsi ya kuyaongeza.

Kabla hatujaona mbinu tano ambazo unaweza kuzitumia kuongeza mauzo kwenye biashara yako naomba nijibu swali muhimu sana ambalo unaweza kuwa unajiuliza, je inawezekana mauzo ya biashara yangu kuongezeka? Jibu ni ndio, haijalishi biashara yako ipo kwenye hatua gani, bado una nafasi ya kuongeza mauzo zaidi ya unayofanya sasa. Kikubwa ni kujua mbinu sahihi za kutumia ili uweze kuongeza mauzo yako.
Kwa kuwa tuko sawa sasa ya kwamba mauzo ya biashara yako yanaweza kuongezeka, sasa unayaongezaje? Hapa ndio zinakuja mbinu tano muhimu unazoweza kutumia kuongeza mauzo yako.

MBINU YA 1; uza bidhaa zinazoendana kwa pamoja.
Mteja anapokuja kununua bidhaa kwako, tayari amejipanga atanunua bidhaa au huduma fulani. Unaweza kumuuzia bidhaa hiyo na akaondoka, unakuwa umepata mauzo ya kile alichotaka na mambo yanaishia hapo. Ila ukiwa mfanyabiashara mjanja unaweza kumuuzia ile bidhaa anayotaka na pia ukamjulisha kwamba kuna bidhaa nyingine ambayo inaweza kutumika kama hiyo. Au kama zikitumika pamoja basi zitaboresha maisha yake kwa kiasi kikubwa.
Kwa mfano kama mtu amenunua nguo muuzie na viatu, na begi la nguo. Kama mtu amenunua kompyuta, mwambie kuna vitu muhimu anahitaji kununua ambavyo vitafanya matumizi ya kompyuta yake kuwa mazuri. Kwa mfano kuweza kuhifadhi data zake sehemu tofauti ili zisipotee kompyuta inapopotea. Kama mtu akinunua kitabu kimoja mwoneshe na vitabu vingine ambavyo vitampatia maarifa zaidi.
Kwenye biashara yoyote unayofanya, kuna bidhaa nyingi unazoweza kuuza kwa pamoja. Fanyia kazi hili.

MBINU YA 2; uza bidhaa yenye uhitaji mkubwa.
Ni rahisi mtu kununua tiba kuliko kununua kinga. Ndivyo binadamu tulivyo, kama hakuna tatizo kubwa linalotusumbua basi hatuhangaiki kutafuta suluhisho.
Ni kazi yako kama mfanyabiashara kuangalia biashara yako vizuri na kuangalia matatizo ya watu, ni matatizo gani ambayo yanawaumiza na wanatafuta sana suluhisho. Kisha wapatie suluhisho la matatizo yao kupitia biashara yako.
Kwa mbinu hii utapata wateja wengi ambao wana matatizo na wanatafuta suluhisho la matatizo yao.

MBINU YA 3; toa punguzo na weka muda wa kuisha kwa punguzo hilo.
Tengeneza aina yoyote ya ofa kwenye biashara yako ila weka muda maalumu ambapo ofa hii itakuwepo. Sio lazima ofa yenyewe iwe kubwa na ya kuathiri biashara yako. Kikubwa ni kutengeneza mazingira ya utofauti kwenye biashara yako ambayo yatamvutia mteja kununua zaidi.
Na unapoweka tarehe ya mwisho wa ofa yako na ukawa unawakumbusha wateja mara kwa mara kwamba ofa inakwisha watasukumwa kufanya maamuzi haraka kabla nafasi hiyo haijaisha.

MBINU YA 4; weka bei zako vizuri.
Bei zako inaweza kuwa sababu ya watu kununua au ikawa kikwazo cha watu kununua. Sio mara zote ukiweka bei ndogo ndio unapata wateja wengi, kuna wakati ukiweka bei kubwa ndio unapata wateja bora zaidi.
Kwa kuwa hili la bei linahitaji mbinu zake pia, tutalijadili kwa undani kwenye makala inayofuata.

MBINU YA 5; boresha huduma unazotoa kwa wateja wako.
Hakuna kitu ambacho kila mtu anapenda kama kupata huduma bora, kama kuona anajaliwa na kama kuona kwamba yeye ni muhimu. Ukijenga biashara yako kwenye misingi hii ya kumjali na kumpatia huduma nzuri mteja wako, mteja ataridhika na hataweza kukaa kimya. Atawaambia wengi zaidi na hivyo utakuwa na wateja wengi na mauzo yako kuongezeka.
Wateja ulionao sasa ni sehemu nzuri sana ya kukuza biashara yako kwa sababu ni wao ambao wataisema biashara yako vizuri. Na pia wanaweza kuwa sehemu ya kuiua biashara yako kama watapata huduma mbovu na kuanza kuisema biashara yako vibaya.
Fanyia kazi mbinu hizi tano na utaona mabadiliko makubwa kwenye mauzo yako. Endelea kusoma makala zangu pamoja na kuwajulisha wengine wasome pia. Karibuni sana.

1 comment:

  1. MBINU ZIMENISAIDIA NIMEANA KUZIFANYIA KAZI NA NINAANZA KUONA MATOKEO ASNTE KUTUKUMBUSHA

    ReplyDelete